NENO LA LEO - MTAZAME ALIYE KARIBU NAWE
Ni jambo la kawaida kuona watu wakihangaika kutafuta msaada juu ya changamoto zinazo wapata. Ndivyo tunashuhudia wengine wanachukua maamuzi magumu hata ya kujiua, baada ya kushindwa kupata msaada. Hebu kila mmoja apige picha, tatizo linapotokea, nani anakuwa wa kwanza kumwendea ili kupata msaada? Wengi watakuambia, ni wazazi, au mume, au mke, au Rafiki, au daktari bingwa, au Mchungaji n.k. kutokana na aina ya tatizo.
Neno la leo linatukumbusha kuwa; mbali na kumtegemea mtu fulani mwenye uwezo wa kukusaidia unapopitia machungu katika maisha haya, Karibu yako yupo Mungu mwenye uwezo zaidi ya wote wanaoweza kutegemewa. Mara nyingi shetani ametudanganya na kututenga na Upendo wa Mungu, na hatimaye akitujeruhi, tunakosa ujasiri wa kuutegemea mkono wa Mungu, macho huwa hayaoni, giza la machungu na simanzi huujaza moyo, na hatimaye wengine, huamua kujiua, wengine huishia kuugua vidonda vya tumbo na shinikizo la damu.
Kumbuka, mwanadamu yeyote sio wa kutegemewa, wakati wowote anaweza kugeuka au hali ikabadilika, wengi wamejeruhiwa na wenzi wao waliokuwa wameijaza mioyo yao, na wameishia kuathirika kwa namna fulani, katika hali kama hiyo ni Mungu pekee aliye Karibu sana na kila mmoja, anaweza kukuokoa katika hali ya kuvunjika moyo.
Unapojeruhiwa na kuumizwa moyo, iwe kwa magonjwa, iwe kwa kuteswa na nguvu za uchawi au majini, iwe kwa kukosa ajira, iwe kwa kushindwa masomo, iwe kwa umaskini, iwe kwa kufiwa na mwenzi, iwe kwa biashara kuporomoka, iwe kuonewa kazini, iwe kwa kukosa mchumba, iwe kwa mwenzi wa ndoa kukutesa kimahusiano, iwe ni kutengwa na marafiki, iwe ni kuonewa na ndugu, iwe ni changamoto yoyote inayo kuumiza na kujeruhi moyo wako; Mungu yuko Karibu nawe KUKUOKOA, mtazame yeye utakuwa salama. Yesu alikufa kwa ajili yetu, ili tuokolewe na kupatanishwa na Mungu Baba, mtazame yeye Uokolewe.
No comments:
Post a Comment